Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniael Chongolo ameahidi kutatua tatizo la uhaba wa watumishi wa Sekta ya Afya katika Wilaya ya Busega. Chongolo ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya siku moja Wilayani Busega tarehe 03 Juni 2022, ambapo aliweza kutembelea ujenzi wa kituo cha Afya Mkula na mradi wa ujenzi wa madarasa 14 ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 katika Shule ya Sekondari Kabita.
“Najua kuna upungufu wa watumishi wa Sekta ya Afya, lakini niseme tu kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kuhakikisha watumishi wanaletwa ikiwemo watumishi wa Sekta ya Afya, lakini tuhakikishe watumishi wanapelekwa kwenye uhitaji na sio kukaa kituo kimoja wakati kwingine kuna uhitaji”, alisema Chongolo.
Katika ziara hiyo Chongolo ametembelea ujenzi wa kituo cha afya mkula ambapo Serikali tayari imetoa kiasi cha TZS milioni 400 kutoka katika Mradi wa Malipo kwa Ufanisi (RBF) na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao utahudumia zaidi ya wakazi 16,000 wa maeneo ya karibu.
Aidha, pamoja na kutembelea miradi hiyo Chongolo alifanya mkutano wa hadhara kwa kusikiliza kero za wananchi katika Kata ya Mwamanyili, ambpo miongoni mwa kero zilizobainishwa na wananchi hao ni pamoja na uvamizi wa viboko katika makazi ya wananchi. Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria anaeleza kwamba tayari kama uongozi wa Wilaya umechukua kuhusu suala hilo kwa kuwasiliana na mamlaka husika na zilifika Wilayani Busega kwaajili ya kutokomeza changamoto hiyo.
Chongolo amezitaka mamlaka zinazohusika na uhifadhi wa wanyamapori kuhakikisha wanadhibiti suala hilo kwani linahatarisha maisha ya wananchi na kupelekea wananchi hao kushindwa kufanya shughuli zao kwa usalama. “Viboko wote ambao wanahatarisha maisha ya wananchi wavunwe ili kuondoa hali hatarishi kwa wananchi”, aliongeza Chongolo.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa