Wilaya ya Busega imeshika nafasi ya pili katika mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kwa ngazi ya Mkoa na kukusanya jumla ya vikombe 8. Mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku 3 kuanzia tarehe 21 hadi 23 Julai 2022 Wilayani Maswa.
Akipokea vikombe vya ushindi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore ametoa pongezi kwa wote waliofanikisha ushindi na kuwataka wafanye vizuri zaidi kwa mashindano mengine hapo mwakani.
Busega imeweza kushika nafasi ya pili, ikiwa nyuma ya Wilaya ya Itilima ambayo imeshika nafasi ya kwanza kimkoa. Aidha, jumla ya wanafunzi 18 kutoka Wilaya ya Busega wamechaguliwa kuunda timu ya Mkoa wa Simiyu ambayo itaenda kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA Kitaifa, huku Busega ikiwa ni Wilaya pekee iliyotoa idadi kubwa ya wanafunzi kwenye timu ya Mkoa wa Simiyu.
Michezo ambayo Busega imeweza kushika nafasi ya kwanza ni pamoja na mpira wa mikono wasichana, riadha wasichana, huku michezo ambayo Busega imeshika nafasi ya pili ni pamoja na mpira wa mikono wavulana, mpira wa miguu wavulana. Kwa upande wa nafasi ya tatu ni mchezo wa mpira wa wavu wasichana, riadha wavulana na fani za ndani.
Kwa upande wake Afisa Michezo wa Wilaya ya Busega Bi. Macklina Ng’itu amesema mashindano ya mwaka huu yalikuwa na upinzani mkubwa ukilinganisha na mwaka jana, hivyo kushindwa kutetea nafasi ya kwanza kama ilivyokuwa mwaka jana, lakini ameahidi kufanya vizuri zaidi katika mashindano mengine ikiwemo mashindano ya UMISETA ambayo yanatarajia kuanza siku za hivi karibuni.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa