Wakulima Wilayani Busega wametakiwa kuongeza thamani ya zao la Pamba kwa kufuata njia bora za kilimo na njia bora za uchakataji pamba kwa kutumia mashine. Hayo yamesemawa na Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Kabuko wakati wa mafunzo ya kilimo cha pamba yaliyofanyika katika kituo cha utafiti wa kilimo Ukiriguru mkoani Mwanza. Katika mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 26 hadi 30 Aprili, 2021 yamehusisha maafisa ugani na wadau wa kilimo kutoka Wilayani Busega.
“Tunataka kufanya mapinduzi ya kilimo cha pamba kwa kuongeza uzalishaji wa kilimo hicho Wilayani Busega, baada ya mafunzo haya tutapita katika kata zetu kutoa elimu ya uzalishaji wa kilimo cha pamba” alisema Kabuko. Katika mafunzo hayo miongoni mwa elimu muhimu waliyoipata washiriki ni pamoja na uongezaji wa thamani wa zao la pamba.
Kwa upande mwingine, Bw. Kabuko amesema licha ya dhamira ya Wilaya kuboresha uzalishaji wa zao la pamba kwa kuongeza uzalishaji, suala la thamani ni kipaumbele katika kulinda maslahi ya mkulima na hivyo halitachukua muda mrefu katika utekelezaji wake. “Ni vyema kuongeza thamani ya pamba, hivyo tunadhamiria kuanza na mashine kwa baadhi ya maeneo machache na baadae kununua mashine za kutosha” aliongeza Kabuko.
Awali, Kaimu Mkurugenzi kituo cha utafiti wa kilimo Ukiriguru Dkt. Henerico Kulembeka, amesema ili kuboresha zao la pamba ni muhimu zao hilo liwe na manufaa kwa wakulima, hivyo ni muhimu kutumia mashine katika uchakataji ili kuongeza thamani ya pamba kwa kupata pamba nyuzi, mbegu, mafuta na mashudu ambayo hutumika kama chakula cha mifugo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe, amewataka maafisa ugani kutumia elimu waliyoipata kuongeza uzalishaji wa zao la pamba ili Wilaya ya Busega iwe mfano wa kuigwa. Pia Mhe. Muniwe amesema ili kuleta ufanisi wa dhumuni la mafunzo hayo ni vyema kushirikiana na vyama vya ushirika na kuhamasisha matumizi ya mashine ya kuchakata pamba ili kutenganisha pamba nyuzi, mbegu, mafuta na mashudu kwa lengo la kuongeza thamani. “Tumekuja kujifunza, na tunaamini tumepata kitu kikubwa na tutafanya mapinduzi makubwa katika kilimo cha pamba katika Wilaya ya Busega” alisema Mhe. Muniwe.
Zao la pamba Wilayani Busega ni miongoni mwa mazao ya biashara yanayolimwa na wakulima wengi Wilayani Busega, lakini uzalishaji wake ni mdogo kwani kwa ekari 1 kwasasa huzalisha kilogramu 175 hadi 200. Hivyo, lengo la mafunzo ni kuhakikisha uzalishaji wa pamba unapanda kutoka msimu mmoja hadi mwingine. Ili kuongeza uzalishaji Bw. Kabuko amesema malengo ya Wilaya ni kuzalisha wastani wa kilogramu 1,200 kufikia mwaka 2024/2025.
Katika mafunzo hayo washiriki wameweza kupata elimu ya kanuni bora za kilimo cha pamba, njia ya kisasa ya uzalishaji wa mbegu za pamba, udhibiti wa magonjwa shambulizi kwa zao la pamba, matumizi ya bora ya mbolea elekezi na uongezaji wa thamani ya pamba. Wadau walioshiriki mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata ina manufaa makubwa katika kilimo cha pamba, hivyo wameomba utekelezaji ufanyike ili kupata matokeo yaliyokusudiwa. Kwa upande wao maafisa ugani, wamekiri kwamba licha ya changamoto zilizopo kweye kilimo cha pamba, lakini kwa kupitia mafunzo hayo wanaamini watafanya kile kinachokusudiwa ili kuleta mapinduzi makubwa kwenye kilimo cha pamba Wilayani Busega.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa