Kikao cha baraza la madiwani robo ya pili Oktoba-Disemba 2019/2020 kimefanyika tarehe 03.04.2020, huku madiwani wakitaka upembuzi wa masuala mbalimbali ikiwemo utendaji wa wakala wa ufundi wa umeme na utengenezaji wa magari ya serikali, TEMESA na utekelezaji wa ujenzi wa stendi ya mabasi ya wilaya ya Busega.
Katika kikao hicho kilichokuwa na wajumbe mbalimbali na madiwani kutoka kata zote 15 na wale wa viti maalum, kilikuwa na hoja na maazimio ya kuleta ufanisi wa masuala mbalimbali katika wilaya ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Busega.
Suala la matengenezo ya magari ya halmashauri ni moja kati ya jambo lililochukua nafasi kubwa miongoni mwa madiwani, ikielezwa utengenezaji wa magari ya halmashauri unagharimu fedha nyingi lakini huchukua muda mfupi kwa magari hayo kuwa na ubovu. Magari ya halmashauri hutengenezwa na TEMESA lakini huchukua muda mfupi kwa magari hayo kuwa na ubovu.
Kaimu Meneja TEMESA Mkoa wa Simiyu, Ramadhan Ally ameeleza kuwa kuna ubovu wa magari unaojitokeza baada ya kumaliza kufanyiwa matengenezo hivyo hupokea tena magari hayo kwa muda mfupi yakiwa yana ubovu mwingine. Hata hivyo baraza la madiwani limeiomba TEMESA kuwa na ufanisi wa utengenezaji wa magari ya halmsahauri huku ikiridhia kama hali haitakuwa na uboreshwaji basi wataomba kutopeleka magari ya halmashauri na kutafuta fundi mwingine kwaajili ya matengenezo ya magari ya halmashauri.
“kwakuwa inaonekana ni kama uzembe, na hilo linatugharimu sana kwa upande wa matumizi ya fedha za halmashauri na kufanya tukose pesa kwa ajili ya shughuli zingine muhimu, hivyo tunaomba TEMESA waboreshe utendaji wao ili kuwa na uhakika wa magari yetu yanapoenda kufanyiwa matengenezo” alisema mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Vumi Magoti. Baraza kwa pamoja liliazimia tija na umuhimu wa uboreshwaji wa utengenezwaji wa magari unaofanywa na TEMESA.
Pamoja na hayo, kwa upande mwingine suala la ujenzi wa stendi ya wilaya lilipata nafasi katika baraza hilo. Stendi ya wilaya ya Busega inayotakiwa kujengwa Nyashimo makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Busega, imeweza kuwa hoja kwenye baraza hilo na madiwani kuomba utekelezaji wake uendane na muda na kwa ufanisi mkubwa kwani ni moja ya chanzo cha kuongeza mapato ya halmashauri.
Mkurugenzi mtendaji wa halmasjauri ya wilaya ya Busega, Anderson Njiginya Kabuko, ameeleza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa stendi ya wilaya ipo kwenye utekelezaji wa hatua mbalimbali na taarifa zitazidi kutolewa kutokana na maendeleo ya ujenzi wake.
Kwa upande mwingine suala la ukusanyaji wa mapato ni moja ya mambo muhimu yaliyotajwa na kusisitizwa kuwa na tija kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri, hivyo ni muhimu kuwa na vyanzo vingi vya mapato. “Mapato ya halmashauri ni muhimu ndio maana tunajitahidi kuwa na mbinu nyingi ili kupandisha mapato yetu, kwa lengo la kukamilisha shughuli mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo inayoendelea na iliyopangwa kutekelezwa” alisema mkurugenzi mtendaji, Anderson Njiginya Kabuko.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa