Madiwani Halamshauri ya Wilaya ya Busega wameitaka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kujiridhisha na takwimu za upatikanaji wa huduma ya maji wilayani Busega. Hayo yamesemwa wakati wa baraza la madiwani robo ya kwanza mwaka wa fedha 2022/2023, lililofanyika tarehe 16/11/2022 katika ukumbi wa Silsos.
Mwakikilishi wa RUWASA, Mhandisi Safiel Senzota alieleza baraza hilo hali ya upatikanaji wa huduma za maji katika Wilaya ya Busega, taarifa ambayo ilionekana kuleta ukakasi kwa baddhi ya madiwani. “Mpaka sasa RUWASA inahudumia wateja wapatao 200,024 ambapo ni zaidi ya asilimia 71 ya wakazi wote, hivyo RUWASA itaendelea kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Busega, ikiwemo upanuzi wa mradi wa maji wa Kiloleli, utekelezaji wa mradi wa maji Nyaluhande na utekelezaji wa mradi wa maji Kabita-awamu ya kwanza”, aliongeza Mhandisi Senzota.
“Tunaomba RUWASA wajiridhishe na takwimu zao kabla ya kuleta taarifa kwenye baraza, na ikiwezekana taarifa hizi ziwasilishwe katika vikao vya kamati za waheshimiwa madiwani ili kuzipitisha kabla hazijaletwa kwenye baraza”, alisema diwani wa Kata ya Igalukilo, Mhe. Charles Lukale. Nae mwenyekiti wa baraza hilo Mhe. Sundi Muniwe, amesema kwamba huduma za maji zimeonekana zikiendelea kuwasumbua wananchi baadhi ya maeneo ndio maana waheshimiwa madiwani wana wasiwasi kwakua wao ndio waliopo karibu na wananchi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amezitaka taasisi za RUWASA na TARURA kuhakikisha wanawashirikisha wameshimiwa madiwani katika utekelezaji wa miradi ili wafahamu miradi hiyo. Aidha, Zakaria amezitaka taasisi hizo kuhakikisha zinawapitisha waheshimiwa madiwani kwenye miradi inayoendelea na iliyokamilika ili wajionee uhalisia wa utekelezaji wa miradi hiyo. “Naagiza RUWASA na TARURA mpange ziara ambazo mtawapeleka waheshimiwa madiwani kujionea kinachoendelea katika miradi mnayotekeleza, ili wajiridhishe na kinachoendelea”, aliongeza Zakaria.
Hali ya upatikanaji wa maji imeboreka ukilinganisha na mitatu nyuma, ambapo Wilaya ya Busega ilikuwa na hali isiyoridhisha ya upatakanaji wa maji, lakini RUWASA na Mamlaka ya maji Busega (BUSEWASA) wamekuwa wakifanya jitihada ambazo kwa mujibu wa taarifa ya RUWASA ambapo inaonesha upatikanaji wa maji ni zaidi ya asimilia 71 , ambapo mahitaji halisi ni zaidi ya lita milioni 7 kwa siku, huku kwasasa upatikanaji ni zaidi ya lita 5.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa