Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema ili bajeti iweze kuwa na ufanisi ni lazima iwe na uhalisia. Zakaria ameyasema hayo wakati wa kikao cha kamati ya ushauri (DCC) Wilaya ya Busega, kilichokuwa na lengo la kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Zakaria amesema ni vyema kuwa na bajeti inayotekelezeka kuliko kuwa na mambo mengi ambayo hayawezi kutekelezeka. “Hatuwezi kuweka kila kitu kwenye bajeti, japo vipaumbele ni vingi, ni vyema kuweka mambo ambayo tunaweza kutekeleza katika kipindi hicho”, aliongeza Zakaria.
Aidha, Zakaria amesema kuna haja kubwa ya Halmashauri kuwa na miradi ya maendeleo ikiwa ni azma ya kuongeza makusanyo ya ndani. “Tunahitaji kuwa na miradi ambayo itakuwa na uzalishaji ambao utasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri”, alisema Zakaraia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Busega, Veronica Sayore amesema kwamba mikakati ambayo Halmashauri imeiweka itatekelezwa kwa awamu kadri makusanyo ya ndani yatakavyokuwa yanapatikana. “Tutatekeleza miradi na shughuli mbalimbali kulingana na mapato ya ndani kadri tutakavyokuwa tunapata fedha”, aliongeza Sayore.
Kwa upande wa wajumbe waliohudhuria kikao hicho wameshauri kwamba ubunifu uongezwe zaidi katika vyanzo vilivyopo na pia kubuni vyanzo vipya ili kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Mapendekezo ya mpango wa bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni TZS 32,397,778,860, ambayo imetokana na vyanzo mbalimbali, ikiwemo ruzuku kutoka Serikali kuu, fedha za wahisani na vyanzo vya mapato vya ndani.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa