Ajali mbaya imetokea alfajiri ya kuamkia leo tarehe 11/01/2022 katika kijiji cha Shimanilwe Kata ya Kabita Wilayani Busega ambapo imehusisha gari ndogo aina Land Cruiser iliyokuwa ikitokea mwanza kuelekea Ukerewe ambayo ilikuwa imebeba waandishi wa habari na gari ndogo ya abiria iliyokuwa inatoka Lamadi kuelekea Mwanza.
Katika ajali hiyo watu 14 wamepoteza maisha na wengine 6 wakiwa majeruhi. Majeruhi 6 walipokelewa kituo cha Afya Nassa na baadae kukimbizwa hospitali ya rufaa Bugando kwa matibabu zaidi.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni pamoja na waandishi wa habari 5, ambao ni Husna Milanzi mwandishi ITV, Abel Ngapemba Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Johari Shani mwandishi Uhuru Digital, Antony Chuwa mwandishi Habari Leo, na Steven Msengi Afisa Habari Ukerewe. Waandishi wa Habari hao walikuwa katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ambapo walikuwa wakielekea Wilayani Ukerewe.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila amefika eneo la ajali na Kituo cha Afya Nassa kutoa pole kwa wafiwa na Majeruhi. Aidha, amesema tukio la ajali hiyo imeleta majonzi kwa mkoa na nchi kwa ujumla. Kafulila amefikisha salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamburi ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kusema kwamba Rais amesikitishwa na ajali hiyo na anawapa pole wote waliopoteza ndugu zao.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria ametoa pole kwa wafiwa wote na kuwaomba Wananchi wa Busega kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu na kusisitiza kwamba Serikali ya Wilaya ya Busega ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.
Miili ya Waandishi waliokuwa wanatokea Mwanza kwenda Ukerewe imepelekwa kuhifadhiwa Hospitali ya Rufaa Bugando kwaajili ya taratibu zingine za mazishi. Wananchi wanaendelea kutambua ndugu zao waliopoteza maisha katika kituo cha Afya Nassa.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa